Fredrick Mulaa ambaye ni mwananchi wa kawaida wa Kenya ameweka kesi katika kitengo cha kupambana na ufisadi cha mahakama kuu kupinga kuondolewa kwa mashtaka dhidi ya aliyekuwa gavana wa Kakamega na ambaye sasa ni waziri Wycliffe Oparanya.
Hatua hii inafuatia uamuzi wa mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP Renson Ingonga wa kumwondolea Oparanya mashtaka ya ufisadi, mkinzano wa maslahi na kujipatia pesa kwa njia ya ulaghai.
Awali tume ya maadili na kupambana na ufisadi nchini EACC ilikuwa imependekeza kushtakiwa kwa gavana huyo wa zamani ikisema kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Oparanya anatuhumiwa kupokea shilingi milioni 56.7 kutoka kwa mwanakandarasi mmoja wa kaunti akiwa gavana wa Kakamega.
Mulaa naye anashikilia msimamo wa EACC akisema kwamba kuondolewa kwa mashtaka hayo kulichochewa na siasa na wala sio maslahi ya umma.
Mulaa ana maswali kuhusu wakati ambao afisi ya DPP ilichagua kuondoa mashtaka hayo ambao ni tarehe 8 Julai 2024 kabla ya Oparanya kuteuliwa kama waziri wa ustawi wa vyama vya ushirika, biashara ndogo na za kadri.
Anahisi hatua hiyo inafanya uadilifu wa afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma utiliwe shaka hasa ikitizamiwa kwamba afisi hiyo haikuonyesha nia ya kuendelea kuchunguza mashtaka dhidi ya Oparanya.
Fredrick anahisi pia kwamba mamlaka iliyomteua Oparanya kuwa waziri ingetilia maanani mashtaka dhidi yake katika mchakato mzima wa kumteua, kusailiwa na bunge na kuapishwa.
Kulingana naye mashtaka hayo yanatosha kumzuia mtu kushikilia wadhifa wowote serikalini.
Katika kujitetea Oparanya alisema kwamba pesa alizopokea ni mkopo kutoka kwa mwanakandarasi huyo na wala sio hongo.