Watu waliokuwa na hasira leo Alhamisi, waliteketeza gari lililomgonga mhudumu wa pikipiki mjini Ruiru, kaunti ya Kiambu katika barabara kuu ya Thika.
Ajali hiyo ilitokea wakati wa dereva wa gari hilo aina ya Toyota Harrier alipokuwa akipita gari jingine kwenye daraja la Ruiru, kabla ya kugonga pikipiki iliyokuwa ikitoka upande mwingine.
Kamanda wa polisi wa Ruiru Alex Shikondi alisema kuwa dereva wa gari hilo alitoroka baada ya ajali hiyo lakini mwendeshaji pikipiki huyo alinusuriwa na kupelekwa kwenye hospitali ya mafunzo na matibabu maalum ya chuo kikuu cha Kenyatta akiwa katika hali mahututi.
Kufuatia kisa hicho wahudumu wa boda boda waliokuwa na hasira waliliteketeza gari hilo lililokuwa na nambari za usajili za Uganda.
Shikondi alishtumu uteketezaji wa gari hilo na kuwataka wananchi kutochukua sheria mikononi mwao akiongeza kusema kuwa kitendo hicho kilicho kinyume cha sheria ni kuharibu ushahidi.