Junet Mohamed, Millie Odhiambo wapendekezwa kuongoza upinzani bungeni

Marion Bosire
2 Min Read

Chama cha ODM kimependekeza Junet Mohamed kuwa kiongozi wa wachache katika bunge la taifa, wadhifa uliosalia wazi baada ya Opiyo Wandayi kuteuliwa kuwa waziri na Rais William Ruto.

Katika taarifa rasmi ya chama iliyotolewa baada ya mkutano wa kamati kuu chini ya uongozi wa Raila Odinga, chama hicho kimeelezea kwamba kinafanya mabadiliko kufuatia uteuzi wa wanachama wake kuhudumu kwa serikali ya Kenya Kwanza.

Millie Odhiambo amependekezwa kuhudumu kama kiranja wa wachache bungeni, Caleb Amisi ameteuliwa kuhudumu kama mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu utathmini wa matumizi ya pesa za umma huku Wilberforce Oundo akiteuliwa kuwa naibu mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu uwekezaji.

Katika taarifa hiyo, chama cha ODM kimeelezea pia kwamba wanachama wake walioteuliwa mawaziri wameshatuma maombi ya kujiuzulu kutoka kwa nyadhifa zao chamani.

Wanachama wa chama hicho watajadiliana kuhusu jinsi ya kujaza nafasi zilizosalia wazi katika uongozi wa chama cha ODM.

Wakati huo huo chama hicho kinasisitiza kwamba hakijaingia kwenye mapatano ya aina yoyote na serikali ya Kenya Kwanza na kwamba chama hicho kitaendelea kuwa katika upinzani kukosoa serikali.

Rais William Ruto aliteua Wycliff Oparanya na Hassan Joho waliokuwa manaibu viongozi wa chama cha ODM, John Mbadi aliyekuwa mwenyekiti, Opiyo Wandayi aliyekuwa katibu wa masuala ya kisiasa na Beatrice Askul Moe mwanachama wa ODM kuwa mawaziri.

Share This Article