Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris – ambaye anatarajiwa kuwa mgombea mteule wa chama cha Democratic katika uchaguzi wa rais wa Novemba – amefanya kile alichokiita “mazungumzo ya wazi na yenye kujenga” na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Akiwa na sauti kali zaidi kuliko Rais Joe Biden, Harris alisema aliweka wazi “wasiwasi wake mkubwa” kuhusu majeruhi huko Gaza, akimweleza Netanyahu kuwa ilikuwa muhimu kwa Israel kujitetea.
“Ni wakati wa vita hivi kumalizika,” alisema baada ya mazungumzo yao ya ana kwa ana katika Ikulu ya White House.
Harris pia alisisitiza juu ya haja ya njia ya suluhisho la serikali mbili, huku akitoa wito kwa Wamarekani kufahamu “suala la utata” juu ya mzozo huo.
Mapema siku ya Alhamisi, Netanyahu alikutana na Biden, ambaye alijiondoa katika kampeni ya kuchaguliwa tena kama Rais wa Marekani siku ya Jumapili.
Mikutano ya Netanyahu katika Ikulu ya White House ilifanyika siku moja baada ya kutoa hotuba kali kwa Congress, akiapa “ushindi kamili” dhidi ya Hamas, huku maelfu ya waandamanaji wanaounga mkono Palestina wakiandamana nje ya bunge.