Rais Joe Biden amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha urais nchini Marekani.
Uchaguzi mkuu nchini humo umepangwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu.
“Wanachama wenzangu wa Democrat, nimeamua kwamba sitakubali uteuzi wa kuwania urais, ila nitaangazia majukumu yangu ya urais katika kipindi kilichosalia cha muhula wangu,” alisema Rais Biden.
Hatua ya Biden inajiri kufuatia miito ya raia wengi wa Marekani kumtaka ajiondoe katika uwaniaji huo, na kumpisha Makamu wa Rais wa Kamala Harris kuwania wadhifa huo.
Kupitia kwa taarifa katika mtandao wa X leo Jumapili, Biden alisema anamuunga mkono Harris kuwania wadhifa huo.
“Leo namuunga mkono kikamilifu Kamala kupewa uteuzi huo. Ni wakati wa kushirikiana pamoja kwa wanachama wa Democrat ili kumshinda Trump,” aliongeza Biden.
Matokeo yake mabaya katika mdahalo kati yake na Trump mwishoni mwa mwezi Juni, yalizidisha shiniko za kumtaka ajiondoe katika kinyang’anyiro hicho kutoka kwa raia wengi wa Marekani, wakiwemo wale wa chama cha Democrat.
Juma lililopita, Biden aligunduliwa ameambukizwa Covid-19, hatua iliyomlazimu kusalia nyumbani.
Macho yote sasa yamekodolewa chama cha Democrat, swali likiwa ni je, Kamala Harris ataidhinishwa kuwania urais kukabiliana na Rais wa zamani Donald Trump?