Azimio yatangaza siku tatu za maandamano kuanzia Jumatano wiki ijayo

Martin Mwanje
1 Min Read

Muungano wa Azimio umebadili mwelekeo na sasa unasema utafanya maandamano kwa siku tatu mtawalia wiki ijayo.

Muungano huo ulikuwa umetangaza jana Alhamisi kuwa utafanya maandamano Jumatano wiki ijayo.

Lakini katika taarifa kwa vyombo vya habari, unasema umefanyia mapitio maamuzi hayo na sasa maandamano yatafanywa siku za Jumatano, Alhamisi na Ijumaa wiki ijayo.

“Kuanzia sasa, maandamano ya amani sasa yatafanyika Jumatano, Alhamisi na Ijumaa wiki ijayo kutokana na maombi mengi kutoka kwa umma ya kuongeza kasi ya maandamano,” ulisema muungano wa Azimio katika taarifa yake.

Hatua hiyo inakuja wakati ambapo serikali imeapa kukabiliana vikali na waandamanaji wanaozua vurugu, kuharibu mali ya umma na kibinafsi na kusababisha maafa kama ilivyoshuhudiwa wakati wa maandamano yaliyoandaliwa na muungano wa Azimio juzi Jumatano.

Akizungumza katika kaunti ya Tharaka Nithi jana Alhamisi, Rais William Ruto alisema hataukubalia muungano huo kujihusisha katika shughuli zitakazosababisha vifo zaidi na uharibifu wa mali.

Muungano wa Azimio umeitisha maandamano kushinikiza serikali kubatilisha sheria ya fedha ya mwaka 2023 na kupunguza gharama ya juu ya maisha.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *