Mswada wa Fedha 2024 uliendelea kukumbana na pingamizi kutoka kila pembe, wa hivi karibuni kuukosoa wakiwa Maaskofu wa Kanisa Katoliki.
Wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofi wa Kanisa Katoliki Nchini, KCCB James Waweru Mwaura, Maaskofu hao wanasema ikiwa mswada huo utapitishwa jinsi ulivyo, basi utawakandamiza Wakenya.
“Ni mtazamo wetu kwamba Mswada wa Fedha 2024, ikiwa utapitishwa jinsi ulivyo, utakuwa kandamizi na kusababisha mateso yasiyoelezeka kwa Wakenya,” walionya Maaskofu hao katika taarifa.
“Ingawa tunafahamu kuwa serikali ina wajibu wa kukusanya kodi ili kufadhili huduma za umma, tuna mashaka mno kuhusu baadhi ya mapendekezo kwenye mswada huo yanayolenga kuongeza ukusanyaji wa mapato. Isitoshe, tunahuzunika juu ya ufisadi uliokithiri katika taasisi zetu za umma na ubadhirifu wa rasilimali za umma kwa shughuli zisizokuwa muhimu.”
Wamelalamikia kuongezwa ushuru thamani wa ziada, VAT kwenye mkate wakisema utafanya maisha kuwa magumu zaidi kwa Mkenya wa kawaida.
Aidha, wamelalamikia ushuru mpya uliopendekezwa kwenye magari wakisema utakuwa mzigo kwa Mkenya wa kawaida kwa kuongeza nauli ya usafiri wa umma.
Mashirika mbalimbali yamepinga Mswada wa Fedha 2024 yakionya kuwa utaongeza ushuru wanaotozwa Wakenya na kufanya maisha kuwa magumu mno.
Kamati ya bunge itakamilisha mchakato wa kupokea maoni kutoka kwa Wakenya leo Jumatatu kabla ya kuandaa ripoti itakayowasilishwa bungeni kwa ama kuzingatia maoni hayo au kuyakataa.
Ni wabunge ambao hatimaye wataamua hatima ya mapendekezo yaliyopo kwenye mswada huo.