Mabingwa wa soka nchini Tanzania, Dar-Young Africans, almaarufu Yanga, wameshindwa kufuzu kwa mechi za nusu fainali ya ligi ya kilabu bingwa Barani Afrika, baada kubanduliwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kupitia mikwaju ya penalti.
Matumaini ya Yanga yalididimizwa baada ya wachezaji Stephane Aziz KI, Dickson Job na Ibrahim ‘Bacca’ Hamad, kushindwa kufunga mikwaju ya Penalti, huku Mamelodi wakitumia fursa zao vyema na kufunga penalti kupitia wachezaji Marcelo Allende, Lucas Ribeiro na Neo Maema.
Timu hizo mbili zilitoka sare tasa katika muda wa kawaida, katika mechi kali iliyochezwa katika uwanja wa Loftus Vers-Feld jijini Pretoria, Ijumaa usiku.
Hata hivyo katika dakika ya 59, bao la Yanga kupitia mchezaji Stephane Aziz KI, lilikataliwa na refa Dahane Beida wa Mauritania, huku wachezaji wakilalamikia vikali uamuzi huo.
Licha ya malalamishi kutoka kwa wachezaji wa Yanga, wasimamizi wa mechi hiyo walishikilia uamuzi wao.
Mamelodi Sundowns sasa itamenyana na mshindi wa mechi ya leo jumamosi usiku kati ya Asec Mimosas ya Kodivaa na Esperance ya Tunisia.