Jose Chameleone asema anaendelea kupata nafuu

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Uganda Joseph Mayanja maarufu kama Jose Chameleone ametoa taarifa kuhusu hali yake ya kiafya ambayo anasema inazidi kuimarika.

Chameleone ambaye amelazwa hospitalini huko Amerika kwa muda sasa, anasema anafurahia mapenzi na uungwaji mkono ambao amekuwa akipata kutoka kwa watu.

“Ninashuruku kwa mapenzi, usaidizi na maombi ambayo nimepokea nikiwa hospitalini. Jumbe zenu za heri njema zimenipa nguvu wakati huu wa changamoto” ilisema taarifa ya mwanamuziki huyo kwenye mitandao ya kijamii.

Alisema pia kwamba anaendelea kupata nafuu huku akishukuru hospitali ya Aline iliyoko Minneapolis pamoja na madaktari na wauguzi ambao anasema wamechangia pakubwa katika safari yake ya kupata nafuu.

“Hata kama kupona kwangu kutagharimu muda na subira, nina uhakika kwamba nitarejelea hali shwari hivi karibuni.” Jose Chameleone aliandika.

Mwanamuziki huyo na kakake aitwaye Humphrey wamekuwa wagonjwa na wamelazwa katika hospitali tofauti huko Marekani.

Baba yao mzazi alithibitisha hayo kwenye mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini Uganda ambapo alisema kwamba wamekuwa wakipitia changamoto si haba kama familia. Alilaumu watu ambao hawatakii familia yake mazuri kwa mabaya yanayowafika.

Website |  + posts
Share This Article