Serikali imetoa shilingi bilion 30.5 ambazo zitagharimia elimu katika shule za sekondari, mikopo ya elimu na ufadhili wa elimu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma kote nchini.
Hii ni kulingana na taarifa ya Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu.
Fedha hizo zinatolewa wakati ambapo wadau katika sekta ya elimu kikiwemo Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari na Vyuo, KUPPET kulalamikia utolewaji wake, hali ambayo ilifanya iwe vigumu kuendesha taasisi mbalimbali za masomo.
Katika taarifa, Machogu ameelezea kwamba kati ya pesa hizo, bilioni 7 zitagharimia masomo katika sekondari msingi za umma huku bilioni 16 zikitumiwa kugharimia elimu ya bure katika shule za sekondari za umma zisizo za malazi.
Taasisi za elimu zitapokea pesa hizo kwenye akaunti zao kabla ya kufunga kwa likizo ya mwezi Aprili wiki ijayo.
Katika kiwango cha elimu ya juu, serikali imetoa shilingi bilioni 6.794 za kutoa mikopo ya kugharimia elimu kupitia kwa bodi ya mikopo ya elimu ya juu – HELB huku bilioni zingine 3.98 zikitengewa ufadhili wa elimu kupitia kwa hazina ya vyuo vikuu.
Kufikia sasa, serikali imetoa shilingi bilioni 32 kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na bilioni 12 kwa ufadhili wa elimu ya juu, mwaka huu wa fedha.
Mwanzo wa mwaka huu, shilingi bilioni 14.4 zilitolewa kugharimia ufadhili wa elimu na mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika vyuo vya umma wanaofadhiliwa na serikali, chini ya mfumo mpya wa kufadhili elimu nchini.