Wanawake 20 katika kaunti ya Kirinyaga watafanyiwa upasuaji wa ugonjwa wa Endometriosis juma hili baada wanawake 60 kufanyiwa vipimo.
Kwa mujibu wa Dkt. Joseph Njagi, ambaye anashiriki shughuli hiyo katika hospitali ya ACK Mt. Kenya eneo la Kerugoya, wagonjwa wanne au watano hufanyiwa upasuaji kila siku.
Dkt. Njagi amesema kaunti hiyo ina madaktari 6 pekee wataalamu wa mfumo wa kike wa uzazi ambao hawawezi kuwahudumia wagonjwa wote ipasavyo kwani kati ya wanawake 10, mmoja anaugua ugonjwa huo. Hali hiyo huwalazimu wagonjwa wengine kutafuta matibabu katika hospitali za kibinafsi.
Vile vile, wagonjwa wengine wametibiwa na madaktari wasio na utaalamu wa ugonjwa huo jambo ambalo limewazidishia masaibu.
Daktari huyo ameiomba serikali kuwekeza katika mpango wa matibabu na uhamasishaji ili kuwanusuru wagonjwa ambao hulazimika kutumia shilingi 350,000 hadi 1,000,000 kufanyiwa upasuaji.
Aidha, amepuuzilia mbali dhana potovu ambapo wanawake wa umri mdogo wamekuwa wakishauriwa kushika mimba kama suluhisho la ugonjwa huo na wengine wakiambiwa kuwa ni uchungu wa kawaida wa hedhi hivyo kuwafanya kuugua kimya kimya.
Hatua hizi za uhamasishaji, kupima na kutibu wagonjwa ni baadhi ya mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo wakati maadhimisho yake yanafanyika mwezi huu wa Machi.
Endometriosis ni ugonjwa unaosababishwa na uwepo wa tishu zinazofanana na ukuta wa ndani wa kifuko cha uzazi sehemu nyingine kwenye mwili.
Dalili zake ni kushindwa kupata ujauzito, kutokwa na damu nyingi ya hedhi au siku za hedhi kuwa nyingi zaidi ya siku 5, maumivu wakati wa haja kubwa au ndogo na maumivu wakati wa kufanya tendo la ndoa.