Mamlaka inayothibiti kampuni za walinzi wa kibinafsi nchini imeagiza kampuni hizo kutia saini mapatano ya kujitolea kulipa angalau kiwango cha chini zaidi cha mishahara kilichowekwa na serikali.
Kwenye waraka kwa wamiliki, wakurugenzi, wanahisa na mameneja wa kampuni za walinzi wa kibinafsi nchini, mkurugenzi mtendaji wa mamlaka hiyo Fazul Mohamed amewapa siku saba kutia saini mkataba huo.
Nakala ya mkataba huo iliyotiwa saini na kuhakikiwa na afisa wa kisheria inafaa kutumwa kupitia barua pepe kwa infor@psra.go.ke.
Muda uliotolewa wa siku saba unaanza leo Jumatatu Januari 29, 2024 na watakaokosa kutekeleza agizo hilo, watachukuliwa hatua ambayo huenda ikaathiri usajili wa kampuni zao.
Kulingana na mamlaka hiyo ya kudhibiti sekta ya walinzi wa kibinafsi PRSA, mlinzi anayelipwa mshahara wa kiwango cha chini kabisa anafaa kupokea shilingi elfu 18,994.08, marupurupu ya nyumba ya shilingi elfu 2,849.11 na elfu 8,156.81 kwa muda wa ziada kazini.
Siku chache zilizopita, chama cha walinzi wa kibinafsi kiliwataka waajiri wao kulipa walinzi kiwango cha chini cha mshahara ambao ni jumla ya shilingi elfu 30.
Katibu mkuu wa chama hicho Daktari Isaac Andabwa, aliitaka serikali ishinikize waajiri wa walinzi wa kibinafsi kutekeleza hilo na kufidia walinzi hao kuanzia siku ambayo agizo la kiwango cha chini cha mshahara lilitolewa.