Mwanamuziki na mwanasiasa Charles Njagua maarufu kama Jaguar amekashifu tabia ya wasanii kugeuka kuwa omba omba baada ya kufuja pesa wanazopata kutokana na kazi zao.
Mbunge huyo wa zamani wa eneo la Starehe kaunti ya Nairo anasema amechoka kusaidia watu hao maarufu kila mara.
Anahimiza wasanii kuwekeza pesa wanazopata kutokana na muziki na kazi nyinginezo za sanaa badala ya kuzitumia kuonyesha maisha wasiyomudu kwenye mitandao ya kijamii.
Jaguar alimtaja mwanamuziki Magix Enga ambaye pia ni mtayarishaji muziki ambaye awali alionyesha mali yake kwenye mitandao ya kijamii na sasa amekuwa fukara na anaomba usaidizi.
Kulingana na Jaguar wasanii wengine wanatapeli watu wenye nia njema ambapo alitaja msanii Mwana Mtule ambaye alikuwa amelazwa katika hospitali ya Kenyatta kutokana na kile alichokitaja kuwa kutiliwa sumu.
Kupitia kwa mchekeshaji Eric Omondi, Mtule alichangiwa pesa nyingi za kugharamia matibabu na baadaye akakiri kwamba hakutiliwa sumu na akaomba msamaha.
Tabia ya wasanii kutowajibika na kuwekeza fedha zao imesababisha Jaguar akome kusajili wasanii zaidi kenye kampuni yake ya Main Switch Production.
Anasema msanii kama huyo akisajiliwa anataka apatiwe makao na mahitaji mengine badala ya kuendesha muziki wake kama biashara ili afaidi.