Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei amewataka Makatibu na Mahasibu serikalini kuzipa kipaumbele hatua za kupambana na ufisadi nchini.
Ametoa wito wakati ambapo serikali ya Kenya Kwanza imeapa kuangamiza ufisadi nchini, ikiwa ni pamoja na katika idara ya mahakama.
Wakati wakihakikisha hilo linatimia, Mkuu wa Utumishi wa Umma amewataka maafisa hao kunadi uongozi mzuri na kukuza utamaduni wa uvumbuzi katika utendakazi wao.
Akiwahutubia wote hao leo Jumatano, Koskei amewataja makatibu na mahasibu kuwa na wajibu muhimu katika kuhakikisha utekelezaji wa maono ya Rais William Ruto kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Amekuwa akikutana na maafisa hao kila mwezi kwa lengo la kukuza ushirikiano wa kimkakati, uvumbuzi na kuangazia changamoto za kitaifa ili kufikia malengo ya ajenda ya mabadiliko ya kiuchumi kuanzia chini hadi juu almaarufu BETA.