Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amewataka wazazi na walezi kuwa katika mstari wa mbele kutoa ushauri kwa wanao wakati huu wa msimu wa Krismasi.
Visa vya utovu wa nidhamu hushamiri wakati wa msimu huo nchini huku baadhi ya watoto wakijiingiza katika uraibu wa kutumia dawa za kulevya.
Ni hali mbayo Waziri wa Elimu anataka ikabiliwe vilivyo kwa wazazi kuingilia kati.
“Nawataka wazazi na walezi kutekeleza mno wajibu wao wa kuwashauri watoto wao ipasavyo juu ya njia za kuepukana na majaribu ambayo huja wakati wa msimu huu wa sherehe,” amesema Machogu.
Waziri amewataka wazazi kuwatadharisha wanao dhidi ya hatari za utumiaji wa dawa za kulevya ambazo matumizi yake yamekithiri katika baadhi ya maeneo ya humu nchini.
Kaunti ya Mombasa ni miongoni mwa zile zinazokabiliwa na changamoto ya dawa za kulevya na mkewe Naibu Rais Dorcas Rigathi ameanzisha kampeni ya kusaidia kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya kote nchini.
Machogu aliyasema hayo alipowahutubia wadau katika sekta ya elimu na kuwashukuru kutokana na mchango wao mwaka unaomalizika wa 2023 ambako marekebisho mbalimbali katika sekta ya elimu yalitekelezwa.