Idara ya utabiri wa hali ya hewa imesema kaunti za Mandera, Wajir, Turkana na Marsabit, zitaendelea kupokea mvua iliyopungua kwa kipindi cha wiki moja ijayo.
Naibu Mkurugenzi wa idara hiyo anayehusika na utabiri Bernard Chanzu, hata hivyo amesema sehemu kadhaa kusini mwa nchi, zitaendelea kupokea mvua kubwa.
Kaunti za Tharaka Nithi, Meru, Kakamega, Kirinyaga, Narok na Migori, pia huenda zikapokea mvua inayoandamana na upepo.
Sehemu za Pwani, Kaskazini Mashariki na Kaskazini Magharibi mwa Kenya zitakuwa na viwango vya joto vya zaidi ya nyuzi 30 wakati wa mchana, wakati sehemu kadhaa katika nyanda za juu mashariki ya Rift Valley, zikinakili kiwango cha chini cha joto cha hadi nyuzi 10.
Hata hivyo, Chanzu alisema kuwa kutokana na mvua kubwa inayoshuhudiwa katika mataifa jirani, huenda kaunti zilizo Kaskazini Mashariki mwa Kenya zikashuhudia mafuriko kutokana na mito kuvunja kingo.
“Sehemu kadhaa za nyanda za juu za Mashariki na Magharibi mwa Rift Valley, eneo la Ziwa Victoria na Kusini Mashariki, zitashuhudia dhoruba na mvua kubwa,” alisema Chanzu.