Wawakilishi wadi wa kaunti ya Meru sasa wanataka afisi ya huduma za jiji la Meru ibuniwe kwa sababu kulingana nao, usimamizi wa kaunti hiyo sasa umeshindikana.
Wakizungumza nje ya majengo ya bunge la kaunti ya Meru baada ya kupokea ombi kutoka kwa wananchi la kufutwa kazi kwa wafanyakazi 12 wa kaunti kwa kutokuwa na uwezo wa kutekeleza kazi zao, wawakilishi wadi hao walisema wanataka Rais aunde afisi ya huduma za jiji la Meru itakayosimamia kaunti hiyo na kuhakikisha huduma kwa wananchi.
Wazo lao linatokana na hali iliyoshuhudiwa katika kaunti ya Nairobi Machi 9, 2020 ambapo Rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta alibuni “Nairobi Metropolitan Service” afisi iliyohamishiwa baadhi ya majukumu ya serikali ya kaunti iliyokuwa ikiongozwa na Gavana Mike Mbuvi Sonko.
Kulingana nao, Gavana Kawira aliombwa na bunge la Seneti aunganishe viongozi wote waliochaguliwa katika kaunti ya Meru lakini hajafanya hivyo mpaka sasa.
Wabunge hao wa bunge la kaunti ya Meru waliahidi kuangazia malalamishi waliyopokea kutoka kwa wananchi na iwapo yanaafiki viwango, watapiga kura kuunga mkono kuondolewa afisini kwa maafisa waliotajwa.
Kuhusu pendekezo la Gavana Mwangaza la kutafuta kuvunjwa kwa serikali ya kaunti ya Meru, wawakilishi wadi hao walisema kwamba wako tayari kurejea kwa wakazi wa kaunti ya Meru ili waamue.
Baadhi ya walalamishi waliozungumza na wanahabari walielezea kwamba maafisa ambao wamewataja kwenye ombi hilo lao ni wale waliotajwa na Gavana Mwangaza katika bunge la Seneti akiwalaumu kwa masaibu yake.