Mahakama kuu imesimamisha kutekeleza kwa ada mpya zilizopendekezwa kutozwa kabla ya kupokea stakabadhi za serikali.
Mnamo siku ya Jumatano wizara ya usalama wa taifa ilichapisha katika gazeti rasmi la serikali ada mpya zikatazotozwa kwa stakabadhi za serikali zikiwemo vitambulisho vya kitaifa, passpoti na stakabadhi nyingine za uhamiaji.
Jaji wa mahakama kuu Lawrence Mugambi, alitoa agizo la kusimamisha utekelezaji wa ada hizo mpya kufuatia ombi lililowasilishwa na daktari mmoja wa upasuaji mwenye makao yake kaunti ya Nakuru Dkt. Magare Gikenyi.
“Agizo limetolewa kusimamisha ilani katika gazeti rasmi la serikali la tarehe sita mwezi Novemba au stakabadhi nyingine ambayo inakusudiwa kutoa amri ya kuongeza au kufanyia mabadiliko ada hizo, hadi kesi kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi iliyowasilishwa,” ilisema semehu ya agizo hilo la mahakama.
Katika ombi lake Gikenyi alidai kuwa ada hizo mpya ni za juu sana na zitawashinda wakenya wengi kulipa.
Gikenyi amemshtaki waziri wa usalama wa taifa Kithure Kindiki, waziri wa fedha Njuguna Ndung’u, bunge la taifa na mwanasheria mkuu.
Jaji Mugambi ameagiza kuwa watatu hao kukabidhiwa nakala za mashtaka katika muda wa siku tatu na wawasilishe majibu katika muda wa wiki moja.
Kesi hiyo itatajwa tarehe 29 mwezi huu.