2Baba atania kuhusu kutoweka kwake

Akizungumza na mashabiki waliohudhuria tamasha lake, 2Baba alisema kwamba alikuwa ametekwa nyara kwa wiki kadhaa.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Nigeria 2Face Idibia au ukipenda 2Baba ameamua kuingiza utani katika suala la kupotea kwake kutoka nyumbani kwao.

Akizungumza na mashabiki waliohudhuria tamasha lake, 2Baba alisema kwamba alikuwa ametekwa nyara kwa wiki kadhaa.

Kuhusu pesa ambazo angechangisha kutoka kwa tamasha hilo, mwanamuziki huyo alisema kwamba zitatumiwa kulipa watekaji nyara wake ili apate uhuru kamili.

Haya yanajiri wiki kadhaa baada ya mama mzazi wa 2Baba kumtangaza kuwa mtu aliyepotea.

Mwanamuziki huyo ambaye jina lake halisi ni Innocent Idibia wa umri wa miaka 49 alitoweka baada ya kutangaza utengano na mke wake Annie Macauley.

Siku chache baadaye alionekana na mpenzi wake mpya Natasha Osawaru. Osawaru alijitetea kuhusu utekaji nyara akisema kwamba 2Baba ni mtu mzima ambaye alichagua kwenda kwake kwa hiari.

Tangazo la 2Baba la kutengana na Annie linaripotiwa kumsababishia matatizo ya kiakili kiasi cha kuwekwa katika kituo cha ushauri nasaha na urekebishaji tabia kwani alikuwa ameingilia unywaji pombe kupita kiasi na matumizi ya mihadarati.

Lakini anaonekana kupata nafuu na amerejea kwenye mitandao ya kijamii ambapo alishukuru ndugu, jamaa, marafiki na mashabiki ambao wamesimama naye.

Alimaliza ujumbe huo kwa jina ‘Annie Macaulay’ na wala sio ‘Annie Idibia’ ishara kwamba sasa amekubali hatima ya ndoa yake.

2Baba alielezea kwamba mchakato wa talaka unaendelea mahakamani.

Website |  + posts
Share This Article