Waziri Kindiki asema juhudi za kuokoa wabunge wawili zimeanza

Marion Bosire
1 Min Read

Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki amesema kwamba kundi la waokoaji limetumwa kuwatafuta na kuwaokoa wabunge na wasaidizi wao waliokuwa wamekwama kwenye mafuriko ya mto Tana.

Wabunge hao Hirbae Said Buya wa Galole na Guyo Ali Wario wa Garsen waliokuwa wakisafiria mashua walionekana kwenye video wakiomba msaada.

Kindiki kwenye taarifa alielezea kwamba mawasiliano yalikuwa yameanzishwa kati ya waokoaji na viongozi hao na watu wengine waliokuwa nao.

Kulingana naye, wahusika wote walikuwa salama na kundi la maafisa kutoka kikosi cha ulinzi wa fuo walikuwa wanaongoza operesheni za kuwaokoa.

Viongozi hao walikuwa wanatoka eneo moja kugawa chakula cha msaada na vifaa vingine na wakapotelea kwenye mto Tana wakitafuta njia ya kuelekea Garsen.

Mwanahabari mmoja ndiye alichapisha video ya viongozi hao wakiomba msaada kwenye mtandao wa X saa nne unusu usiku.

Walikuwa kwenye mashua ambapo mmoja wa watu waliokuwamo alielezea kwamba waliondoka Mnazini saa kumi alasiri kuelekea Garsen lakini wakapotelea kwenye mto huo wa Tana.

Share This Article