Aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amesema kwamba raia wa nchi hiyo wanamwamini kwa kiwango kikubwa ndiposa aliamua kuwania Urais kwenye uchaguzi mkuu wa Mei 29, 2024.
Hata hivyo mahakama ya upeo nchini humo ilimzuia kuwania wadhifa huo na kushikilia wadhifa wa ubunge kutokana na kile ilichokitaja kuwa hukumu iliyotolewa dhidi ya kiongozi huyo ya kifungo cha miezi 12 gerezani kwa makosa ya ufisadi.
Lakini katika mahojiano na shirika la BBC, Zuma alipinga uamuzi huo akisema kwamba hakuna shtaka dhidi yake lililodhibitishwa.
Zuma alikosana na mrithi wake Cyril Ramaphosa na akaamua kubuni chama kwa jina “uMkhonto we Sizwe -MK” ambacho amekuwa akipigia debe. Jina la chama hicho ndilo jina lililopatiwa kundi la wapiganaji la chama tawala ANC wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi.
Bado Zuma wa umri wa miaka 82, ana uungwaji mkono wa kiwango cha juu hasa katika mkoa alikozaliwa wa KwaZulu-Natal.
Tume ya uchaguzi nchini Afrika Kusini imeamua kwamba picha ya Zuma itasalia kwenye karatasi za kupigia kura kwa sababu yeye ndiye kiongozi aliyesajiliwa wa chama cha upinzani cha uMkhonto we Sizwe -MK.
Jina lake hata hivyo litaondolewa kwenye orodha ya wabunge wateule wa chama hicho.
Wawaniaji wakuu wa Urais kwenye uchaguzi huo wa wiki ijayo ni pamoja na Rais wa sasa Cyril Ramaphosa, Julius Malema wa chama cha EFF na John Steenhuisen wa chama cha DA.