Zimbabwe yaunga mkono azma ya Raila kuwania uenyekiti wa AUC

Tom Mathinji
1 Min Read
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa.

Azma ya kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga ya kuwania uenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika AUC, imepigwa jeki baada ya Zimbabwe kuunga mkono azma hiyo.

Hayo ni kulingana na Rais William Ruto ambaye ameishawishi Zimbabwe kuchukua hatua hiyo, huku akifanya ziara ya siku mbili ya kiserikali nchini humo.

Kenya imewasilisha mgombea wake kwa wadhifa huo kwa kipindi cha mwaka 2025-2028.

Haya yanajiri huku baraza kuu la Muungano wa Afrika, lilikiafikia uamuzi kwa kauli moja mnamo tarehe 15 mwezi Machi mwaka huu kwamba eneo la Afrika Mashariki liwasilishe wagombezi wa wadhifa huo.

Rais aliyasema hayo leo Jumamosi katika ikulu ya Bulawayo nchini Zimbabwe aliposhauriana na mwenyeji wake Emmerson Mnangagwa.

Wakati wa mashauriano hayo Kenya na Zimbabwe zilitia saini mikataba tisa ya maelewano katika sekta za miundombinu, afya, elimu, ulinzi, biashara na uwekezaji miongoni mwa sekta nyingine.

Share This Article