Makubaliano ya fedha yenye thamani ya shilingi bilioni 350 yametiwa saini wakati wa ziara ya Rais William Ruto nchini Japani.
Makubaliano hayo yatasaidia miradi na mipango katika sekta ambazo zinalenga kuleta mabadiliko ya kiuchumi humu nchini.
Miradi mikubwa ambayo itanufaika ni mfumo ikolojia wa muundombinu wa Dongo Kundu na daraja la Mombasa Gateway huko pwani kwa thamani ya shilingi bilioni 260.
Rais Ruto na Waziri Mkuu Fumio Kushida pia walikubaliana kwamba Kenya itatoa dhamana ya Samurai ya shilingi bilioni 40 nchini Japani kufadhili miradi ya nishati na miundombinu.
Dhamana ya Samurai ni ya sarafu ya yeni inayotolewa jijini Tokyo na kampuni moja isiyokuwa ya Japani. Hata hivyo, dhamana hiyo inadhibitiwa na sheria za Japani.
Kenya pia imepata shilingi bilioni 30 kutoka kwa Benki ya Japani ya Ushirikiano wa Kimataifa ili kununua mashine.
Shilingi bilioni 15 zitatolewa kwa mradi wa maendeleo ya mvuke wa Olkaria. Japani pia itatoa shilingi bilioni moja za uzalishaji wa oksijeni ya kutumiwa kwa utoaji wa matibabu katika hospitali mbalimbali.
Kupitia Umoja wa Mataifa, Kenya itapokea shilingi milioni 320 za msaada wa kibinadamu kwa ajili ya wale walioathiriwa na mafuriko ya hivi karibuni yaliyosababishwa na mvua za El Nino.
Rais Ruto alishuhudia kutiwa saini kwa makubaliano ya pande mbili leo Alhamisi baada ya kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio.
“Baada ya mazungumzo ya kina na Waziri Mkuu juu ya ushirikiano kati ya Kenya na Japani, nina imani kuwa uhusiano wetu wa pande mbili utasalia thabiti,” alisema Rais Ruto.
Makubaliano mengine ni pamoja na mikataba ya maelewano katika sekta za tekonolojia na mawasiliano, afya, fedha na usalama.
Alisema mikataba hiyo itajumuisha uongezaji wa uwezo wa Taasisi ya Utafiti wa Matibabu nchini Kenya, KEMRI kujenga uwezo wake wa usimamizi wa majanga kwa gharama ya shilingi bilioni 3.
Ili kuimarisha uhsirikiano kati ya nchi hizo mbili katika ulinzi, makubaliano juu ya ushirikiano wa ulinzi pia yalitiwa saini.
Hii inaifanya Kenya kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kutia saini makubaliano ya ulinzi na Japani.
“Hii itatuwezesha kufanya kazi pamoja katika kuhamasisha amani na uthabiti barani Afrika na njia zote za biashara baharini,” aliongeza Rais Ruto.
Rais pia alipongeza usaidizi wa Japani kwa ukamilishaji wa awamu ya pili ya Mpango wa Unyunyiziaji Maji Mashamba wa Mwea na Mpango wa Kitaifa wa Mchele.
Viongozi hao wawili pia walijadili hali ya usalama katika upembe wa Afrika, eneo la maziwa makuu na nchini Haiti.