Zelenskyy amtaka Trump kumaliza vita Ukraine

Marion Bosire
1 Min Read

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amemtaka Rais wa Marekani Donald Trump apatanishe makubaliano ya kusitisha vita katika nchi yake vinavyoendelezwa na Urusi.

Zelenskyy alisema haya jana Jumamosi huku akisifia juhudi za Trump zilizosababiisha kuafikiwa kwa makubaliano ya kumaliza mapigano katika ukanda wa Gaza akisema vita vingine vinaweza pia kukomeshwa.

Zelenskyy anataka Trump amshinikize Rais wa Urusi Vladimir Putin, akubali mazungumzo ya kukomesha vita katika nchi yake.

Zelenskyy na Trump waliwasiliana kwa njia ya simu jana Jumamosi ambapo alitoa ombi hilo, siku moja tu baada ya Urusi kuanzisha mashambulizi ya kiwango cha juu dhidi ya Ukraine.

Mashambulizi hayo yalilenga vyanzo vya umeme na kusababisha sehemu za jiji kuu Kyiv na maeneo mengine tisa ya nchi hiyo kukosa umeme lakini kufikia sasa huduma za umeme zimerejeshwa.

Juhudi za kidiplomasia za kumaliza mwingilio wa Urusi nchi Ukraine zimepungua katika wiki za hivi karibuni hali inayoaminika kutokana na hatua ya wengi kuangazia makubaliano ya kusitisha vita vya Israel huko Gaza.

Trump aliyetangaza awamu ya kwanza ya mpango wa kusitisha vita kati ya Israel na Hamas Jumatano, alikutana na kiongozi wa Urusi Vladimir Putin Agosti kwa majadiliano lakini hawakuafikiana kuhusu kusitisha vita.

Website |  + posts
Share This Article