Mwanamitindo wa asili ya Uganda Zari Hassan na mume wake Shakib Cham Lutaaya wamepatana tena baada ya sintofahamu ya muda iliyoibuliwa na Zari mwenyewe.
Zari na Shakib wameamua kutupilia mbali matatizo ya ndoa yaliyokuwa yakizungumziwa sana hadharani, baada ya kuungana tena nchini Uganda katika kile kinachoonekana kuwa maridhiano ya furaha na yaliyojaa bashasha.
Wawili hao walionekana wakifurahia pamoja, wakitania na kucheka kwa pamoja, hali tofauti kabisa na mvutano uliotanda katika uhusiano wao baada ya Zari kutangaza hadharani wiki chache zilizopita kuwa ndoa yao ilikuwa imefikia mwisho.
Shakib pia alitania kuhusu tangazo hilo la kushtua, akimuuliza kwa mzaha mke wake kilichokuwa kimempata na kusababisha atangaze hilo.
“Nini kilikupata? Ulikuwa umepagawa? Huenda kuna nguvu fulani kichwani mwako zinazozungumza na wewe, na usipokuwa na Mungu, unaweza kupotea,” alisema Shakib.
Aliendelea kwa kumkumbusha Zari kuhusu msimamo aliowahi kuutangaza hadharani kuhusu ndoa yao.
“Nadhani unaitaka ndoa hii, na uliwahi kutangaza hadharani kwamba huu ndio uhusiano wako wa mwisho. Mungu alisikia na kujibu maombi yako, kwa hiyo huendi popote.” Shakib alimwambia Zari.
Mashabiki kwenye mitandao ya kijamii tangu wakati huo wamekaribisha kwa furaha kurejea kwa wawili hao, wakieleza kufurahishwa na ukweli kwamba wamepatana tena baada ya tofauti zao za hivi karibuni.