Zamu hii ninajua hatarudi asema Ida Odinga akimwaga mumewe

Marion Bosire
2 Min Read

Mjane wa waziri mkuu wa zamani Raila Amolo Odinga amesema kwamba anafahamu kwamba mume wake zamu hii hatarejea ni yeye atajiunga naye alikokwenda.

Akihutubia waombolezaji katika hafla ya mazishi ya Raila Odinga huko Bondo, Mama Ida alisema kwamba Raila ambaye alikuwa mpiganiaji uhuru alikuwa akikamatwa au kwenda mafichoni mara nyingi na kilamara alijua kwamba angerejea lakini sio zamu hii.

Kulingana naye, miaka ya kukamatwa au kujificha ya maisha ya Raila ilikuwa mtihani mkubwa kwa familia yao.

Mama Ida alimshukuru Rais William Ruto kwa kuwa mwaminifu kwa maneno yake ya kumpa Raila mazishi ya kipekee akisema kwamba katika eneo la Bondo, hawajawahi kuona mazishi ya kiwango hicho.

Alitaja pia watu waliosimama na familia yake akiwataja kuwa marafiki wa ukweli wakiongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, rafiki ya Raila wa dhati Olesegun Obasanjo na mjane wa marehemu waziri mkuu wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai.

Kutokana na wingi wa marafiki hao, Mama Ida aliahidi kuwaandikia waraka wa shukrani baadaye kwani hangeweza kuwataja wote.

Mama alisimulia jinsi ilikuwa vigumu kwa Raila kuendeleza maisha yake katika kiwango cha familia na katika kiwango cha kiongozi lakini alijibidiisha.

Alifichua kwamba kando na mkewe na watoto wake, Raila alimpenda sana ndugu yake Seneta wa Siaya Oburu Odinga na iwapo yeyote angetaka chochote kutoka kwa Raila angepitia kwa Oburu ili kuhakikisha kwamba anapata anachokitaka.
Mwili wa Raila utazikwa leo jioni nyumbani kwake, Kang’o ka Jaramogi, Bondo kaunti ya Siaya.

Website |  + posts
Share This Article