Yul na Linc Edochie wazika tofauti zao

Wana hao wa Pete Edochie wanaonekana kwenye video wakikumbatiana kwa furaha.

Marion Bosire
1 Min Read

Waigizaji wa Nollywood ambao ni kaka Yul Edochie na Linc Edochie, hatimaye wamezika tofauti zao katika kaburi la sahau.

Ndugu hao wawili ambao ni wana wa mwigizaji nguli Pete Edochie walitofautiana awali kuhusu ndoa ya Yul na mke wake wa pili kwa jina Judy Austin.

Tatizo lilianza pale ambapo Linc alizungumzia kutofurahishwa kwake na jinsi Yul alikuwa akimtangaza Judy mitandaoni bila kujali hisia za mke wake wa kwanza May.

Alipohojiwa kwenye kipindi cha mitandaoni cha mwigizaji mwenza Kanayo o Kanayo mwezi Novemba mwaka 2024, Linc alisema kila mtu ana haki ya kuishi maisha yake apendavyo lakini iwapo anayoyafanya yanaathiri wengine ni bora kuwaza tena.

Usemi wa Linc kwenye mahojiano hayo ulighadhabisha Yul ambaye alitumia mitandao kumfokea yeye pamoja na aliyekuwa akimhoji akiwataja kuwa washenzi.

Sasa Yul ametangaza kupitia mitandao kwamba yeye na kakake mkubwa Linc wamesuluhisha tofauti zao, suala ambalo wengi wa wafuasi wake mitandaoni wamelifurahia.

Alichapisha video inayomwonyesha yeye ya Linc wakikumbatiana baada ya kupeana salamu za kitamaduni na kuandika, “Kuungana upya kwa ndugu. Damu ni nzito kuliko maji.”

Haya yanajiri siku chache tu baada ya baba ya wawili hao kutimiza umri wa miaka 78. Pete Edochie alizaliwa Machi 7, 1947.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *