Msanii wa muziki nchini Uganda Wycliff Tugume maarufu kama Ykee Benda ametangaza kwamba amerejelea muziki, baada ya kuondokea tasnia hiyo kwa muda.
Benda amesema kwamba sasa yuko tayari kutuliza kiu ya mashabiki wake kwa kazi mpya aliyoipa jina la ‘Tempting’.
Kupitia mitandao ya kijamii, Ykee Benda alifichua kuwa aliamua kutokuwepo kwenye muziki makusudi kwani alihitaji mapumziko ili kushughulikia maisha yake binafsi.
“Samahani nimechukua muda mrefu, lakini tafadhali nivumilieni, nilihitaji mapumziko kutoka katika ulimwengu huu wa muziki, kujihuisha upya,” alisema msanii huyo.
Aliongeza kwamba kwa muda ambao amekuwa kimya, amepoteza marafiki kadhaa, amepata wengine wapya, amepata mapenzi na sasa anajenga familia, amepoteza pesa na pia amepata kiasi fulani.
“Lakini muhimu zaidi, mapumziko haya yalikuwa kuhakikisha sipotezi nafsi yangu, na namshukuru Mungu sikufanya hivyo,” aliongeza.
Akizungumzia muziki wake mpya, Ykee Benda anaamini kuwa ‘Tempting’ ni kile hasa ambacho mashabiki wake wanastahili.
“Sasa niko tayari kuwapa kile mnachostahili. TEMPTING itawaletea sauti tulivu, yenye mdundo mzuri, na itasikika mpya kabisa masikioni—inakuja hivi karibuni. Asanteni kwa uvumilivu wenu,” alimalizia.
Ykee Benda wa umri wa miaka 34 sasa, alijipatia umaarufu mwaka 2016 alipotoa nyimbo kama Muna Kampala na marudio ya wimbo Farmer na anafahamika pia kwa uwezo wake wa kuimba mitindo mbali mbali kama Afrobeats, R&B na dancehall.