Yahya Sinwar atangazwa kiongozi mpya wa Hamas

Tom Mathinji
1 Min Read
Yahya Sinwar,atajwa kiongozi mpya wa Hamas.

kundi la Hamas limemtangaza Yahya Sinwar kuwa kiongozi wake wa kisiasa, baada ya kuuawa kwa Ismail Haniyeh jijini Tehran, nchini Iran Julai 31,2024.

“Kundi la Hamas linatangaza kuteuliwa kwa kamanda Yahya Sinwar kuwa kiongozi wake wa kisiasa na kuchukua mahala pa marehemu Ismail Haniyeh,” ilisema taarifa kutoka kwa Hamas.

Sinwar mwenye umri wa miaka 61 ametajwa na Israel kuwa alihusika katika kupanga shambulizi la Oktoba 7, 2023 katika himaya ya Israel ambapo watu 1,200 waliuawa na zaidi ya 200 kuchukuliwa mateka.

Tangu mwaka 2017, Sinwar amehudumu kama kiongozi wa Hamas katika ukanda wa Gaza, na kuteuliwa kwake kuwa kiongozi mkuu wa Hamas, kulijiri baada ya mashauriano ya kina yaliyoandaliwa Jijini Doha nchini Qatar.

Uteuzi wa Sinwar unajiri huku taharuki ikiendelea kutanda Mashariki ya Kati, huku Iran na washirika wake wakitishia kulipiza kisasi baada ya kuuawa kwa Haniyeh, ambapo Israel imelaumiwa kwa kutekeleza mauaji hayo.

Hata hivyo, Israel haijasema lolote kuhusu kuuawa kwa Ismail Haniyeh.

Share This Article