Mwigizaji wa filamu za Bongo Jackline Wolper ametangaza kwamba yeye na Rich Mitindo ambaye amekuwa mume wake na baba ya watoto wake, wameachana.
Wolper alifichua hayo alipokuwa akijibu mashabiki na wafuasi wake ambao wamekuwa wakimtumia picha na video ambazo huenda zikawa za mienendo ya Rich.
“Hello Mashabiki zangu, marafiki na Watanzania wote mnao nitakia mema. Ni kwa masikitiko mengi sana mmekuwa mkinitumia message, links, na Clips mbalimbali, huku mkinishauri, kuniombea na kunitia moyo.” alianza Wolper.
Alikiri kupokea jumbe zao na kuwashukuru wema na wabaya akiwaondolea wasiwasi kuhusu furaha na amani ya moyo wake kwani wameshatengana.
Mama huyo wa watoto wawili amesema anaendeleza mchakato wa talaka na hivyo kuwataka wanaompelekea maneno kuhusu Rich ambaye anamrejelea kama mzazi mwenzake, wakome.
Alisema Rich ambaye anahusika na biashara ya mitindo ya mavazi yuko huru “kufanya chochote kinacho mpendeza”.
Katika Insta Stories, Rich amechapisha video inayomwonyesha akijiburudisha katika eneo fulani na kuandika, “Maisha ni mafupi sana, furahikia muda ulionao.”
Alionya pia kina dada waache kumsumbua akisema kwamba bado hajampa talaka Wolper.
Wolper na Rich Mitindo walifunga ndoa Novemba 19, 2022 na kufikia sasa wamebarikiwa na watoto wawili, wa kwanza wa kiume na wa pili wa kike.
Mtangazaji Burton Mwemba maarufu kama Mwijaku hata hivyo anahisi kwamba ni kiki tu akisema Wolper na Rich kamwe hawawezi kutengana.
Wolper tayari amemjibu Mwijaku akisema yeye sio wa kutafuta kiki na kumtishia kumchukulia hatua za kisheria.