Wizara ya Utalii yalenga kuwavutia watalii milioni 5 kufikia 2027

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa Utalii Rebecca Miano.

Waziri wa Utalii na wanyamapori Rebecca Miano, amesema wizara yake inalenga kuongeza idadi ya watalii wanaozuru hapa nchini hadi milioni tano, kufikia mwaka 2027, kutoka idadi ya sasa ya watalii milioni 2.1.

Akizungumza alipokutana na maafisa kutoka chama cha utalii na kile cha kuwaelekeza watalii, Miano alisema ushirikiano na washirika mbali mbali utasaidia taifa hili kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 352 zinazokusanywa sasa hadi shilingi bilioni 824 kila mwaka.

“Kujitolea kwangu kunalenga kubuni ushirikiano na sekta ya kijamii ili kuwa na mtazamo sawa katika kufanyia mageuzi sekta ya utalii, ili iwe nambari moja katika kuleta mapato, kubuni nafasi za ajira na ukuaji wa pato jumla la taifa,” alisema Miano.

“Kama wizara, tunapongeza sekta ya kibinafsi kwa kuwa mwenyeji na kushiriki katika hafla za hapa nchini na Kimataifa, kuhamasisha kuhusu sera, kuendeleza ubunifu wa bidhaa za kitalii na usambazaji wa habari kuhusu soko la utalii,” aliongeza Miano.

Aidha waziri huyo alisema wizara hiyo iko katika harakati za kubuni mkakati wa kitaiofa wa kupigia debe utalii wa hapa nchini.

“Tutashirikiana kubuni bei nafuu za usafiri na malazi ili kukuza utalii wa hapa nchini,” aliongeza waziri Miano.

Miano alisema wizara yake itatumia fursa ya siku ya kimataifa ya Utalii Septemba 27, 2024, kupigia debe utalii wa nyumbani.

Maeneo mengine ambayo waziri huyo alidokeza watashirikiana na sekta ya kibinafsi ni pamoja na kufanya sekta hiyo kukumbatia dijitali, na ufadhili ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo.

TAGGED:
Share This Article