Uzalishaji wa mahindi hapa nchini umeongezeka kwa asilimia 43, wakati wa msimu wa upanzi wa mwaka 2023.
Ufanisi huo umetajwa kuchochewa na utekelezwaji kikamilifu wa mpango wa usambazaji mbole za gharama nafuu kote nchini.
Akizunumza leo Ijumaa alipofungua rasmi maonyesho ya kilimo ya kaunti ya Kisumu, katibu katika wizara ya kilimo Dkt Kipronoh Ronoh, alisema katika kipindi hicho magunia milioni 60,2 ya kilo 90 ya mahindi, yalizalishwa wakati wa msimu wa mvua za vuli na masika.
“Katika kipindi cha uzalishaji cha mwaka 2023, jumla ya magunia Milioni 60.2 ya kilo 90 ya Mahindi yalizalishwa. Vile vile katika kipindi hicho takriban magunia Milioni 7.14 ya kilo 90 ya maharagwe na magunia milioni 4.89 ya kilo 90 ya ngano yalizalishwa.” alisema Ronoh.
Kuhusu mafuta ya kupikia, katibu huyo alisema serikali inalenga kuongeza eneo la ukuzaji mazao yanayozalisha mafuta ya kupikia kutoka hekari 60,000 hadi ekari 450,000 nakupunguza uagizaji mafuta ya kupikia kutoka nje kwa asilimia 50.
Alisema idadi ya watu wanaokumbwa na changamoto ya usalama wa chakula imepungua kutoka watu milioni 2.7 mwezi Julai mwaka 2023,hadi watu milioni 1.9.
Kulingana na katibu huyo, serikali itasambaza magunia milioni 12.5 za mbolea ya gharama nafuu kwa wakulima katika wadi zote 1,450 nchini, ili kuimarisha zaidi uzalishaji wa chakula.