Wizara ya Kilimo na Baraza la Magavana (CoG) zimeazimia kuboresha ushirikiano kati ya serikali kuu na zile za kaunti ili kuifanyia mabadiliko sekta ya kilimo.
Azimio hilo limefikiwa wakati wa mkutano wa siku mbili wa ngazi ya juu kati ya Wizara ya Kilimo na CoG uliofanyika katika hoteli moja mjini Mombasa.
Waziri wa Kilimo Andrew Karanja, akizungumza wakati wa hafla ya ufungaji wake, amesema mkutano huo ulisisitiza umuhimu wa serikali kuu na zile za kaunti kuimarisha mikakati inayolenga kuifanyika mabadiliko sekta ya kilimo nchini kwa lengo kuimarisha uchumi na kuongeza mapato ya wakulima.
Hoja kuu zilizojadiliwa wakati wa mkutano huo ni pamoja na utekelezaji wa Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi kuanzia Chini hadi Juu (BETA) katika sekta ya kilimo, utekelezaji wa mpango wa mbolea ya bei nafuu na ufufuaji wa huduma za nyanjani miongoni mwa zingine.
Waziri Karanja amesema kufuatia majadiliano ya kina, ilikubaliwa kwa kauli moja kuwa ngazi hizo mbili za serikali zitafanya mashauriano ya mara kwa mara ili kukuza mtazamo madhubuti na ulioratibiwa wa kuifanyia sekta ya kilimo mabadiliko.
Alidokeza kuwa Kongamano kati ya Ngazi zote za Serikali juu ya Kilimo (IGF-A) linaloteja pamoja washikadau wakubwa katika sekta ya kilimo litafanyika Februari 2025 mwakani.
“Wizara na serikali za kaunti zitatekeleza Mkakati wa Pamoja wa Mashauriano na Ushirikiano katika Sekta ya Kilimo (JASCCOM) ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa JASCCOM, kamati ongozi ya pamoja ya miradi yote,” aliongeza Waziri.
Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi, ambaye pia ni mwenyekiti wa CoG, alisema serikali za kaunti kwa ushirikiano na Wizara ya Kilimo zitahakikisha upitiaji upya na ujumuishaji wa hatua na malengo ya mpango wa serikali kuu wa BETA katika Mipango ya Pamoja ya Maendeleo ya Kaunti (CIDP) huku kukiwa na malengo bayana ya kaunti yaliyoainishwa kwa kila kaunti.
Aliongeza kuwa kikosi kazi cha pamoja kitaundwa ili kusimamia ujumuishaji wa BETA katika CIDP.