Katibu katika Wizara ya Kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh amesema serikali imejitolea kuipiga jeki sekta ya kilimo kuhakikisha taifa hili lina utoshelevu wa chakula na kuimarisha maisha ya Wakenya.
Dkt. Ronoh aliyasema hayo alipoongoza hafla ya kufuzu kwa vijana 210 watakaopiga jeki kilimo biashara na ambao watatoa mafunzo kwa wakulima kuhusu mbinu za kisasa za kilimo.
Alisema vijana hao, waliotoka katika kaunti ya Kericho, ni sehemu ya watu wengine 2,500 ambao wako tayari kubadilisha mustakabali wa kilimo hapa nchini.
“Kwa kufanya kazi kwa karibu na wakulima,vijana hawa wa kilimo biashara watatekeleza jukumu muhimu kwa kufanya maamuzi yanayozingatia ukusanyaji wa data, kufanikisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa bei nafuu na kuimarisha huduma za nyanjani za kilimo,” alisema Dkt. Ronoh.
Katibu huyo alikariri kujitolea kwa serikali kuendelea kuwaunga mkono wakulima wadogo wadogo, kwa kuhakikisha sauti zao zinasikika na maswala yao yanashughulikiwa ipasavyo.
Dkt. Ronoh alisema vijana hao waliofuzu, wamepewa nafasi bora ya kuchangia ufanisi wa sekta ya kilimo hapa nchini.
Katika hafla hiyo, Katibu huyo alikuwa ameandama na Gavana wa Kericho Erick Mutai, yule wa Nandi Stephen Sang na maafisa wakuu wa serikali ya taifa na kaunti miongoni mwa viongozi wengine.
Aidha, Dkt. Ronoh alitoa wito kwa Wakenya kujisajili kwa mpango wa afya wa SHA, kuhakikisha wanapata huduma za afya katika vituo vya afya.