Wizara ya Fedha yapunguza bajeti ya chakula kwa wanafunzi shuleni

Marion Bosire
1 Min Read

Wizara ya Elimu imeambia kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Utekelezaji kuwa fedha za kufanikisha mpango wa lishe shuleni zimepunguzwa kwa shilingi bilioni 2.4 katika bajeti ya Mwaka wa Fedha wa 2024/2025.

Akizungumza alipofika mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na mbunge wa Budalangi Raphael Wanjala, Katibu katika Wizara ya Elimu Dkt. Belio Kipsang alifichua kwamba mpango huo umekuwa ukipata mgao wa ziada kwa bajeti isipokuwa kwa Mwaka wa Fedha wa 2024/2025.

Dkt. Kipsang alielezea kuwa mpango huo ulipokea shilingi bilioni 1.96 katika Mwaka wa Fedha wa 2022/2023 na shilingi bilioni 5.4 katika Mwaka wa Fedha wa 2023/2024. Hata hivyo, katibu huyo alielezea wabunge kuwa fedha zilizotengewa mpango huo sasa ni shilingi bilioni 3.

Mbunge wa Marakwet Magharibi Timothy Kipchumba, alisikitika na kuuliza sababu ya kupunguzwa kwa bajeti ya mpango wa lishe shuleni, huku akionya kuwa kupunguzwa kwa fedha za mpango huo kunaweza kusababisha kupungua kwa chakula.

Wizara ya Elimu iliihakikishia kamati hiyo kuwa watashauriana na maafisa mbalimbali husika katika Wizara ya Fedha ili waweze kupata mgao wa ziada.

Kufikia sasa, wizara hiyo inasema mpango wa lishe shuleni unafaidi watoto milioni 2.6 wengi wao wakitoka katika maeneo yanayokumbwa na ukame, huku wengine wakitoka familia maskini.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *