Wizara ya Fedha inatafuta mbinu mbadala za ushirikiano baina ya serikali na sekta za kibinasfi maarufu kama PPP ili kufadhili miradi mikubwa ya miundombinu.
Hatua hiyo inafuatia kusitishwa kwa mkataba wa Adani uliodhamiria kusaidia katika upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA na ujenzi wa laini za kusambaza umeme kupitia makubaliano yaliyofikiwa kati ya kampuni ya Adani na ile ya kusambaza umeme nchini ya KETRACO.
Katibu wa Wizara hiyo Dkt Chris Kiptoo amesema kuwa serikali haina uwezo wa kifedha kufadhili miradi ya maendeleo kama vile upanuzi wa JKIA .
Katibu huyo ameongeza kuwa walipa ushuru tayari wamelemewa na mzigo wa ushuru unaotozwa kwa sasa.
Akizungumza alipofika mbele ya Kamati ya Bunge ya Uhasibu wa Pesa za Umma jana Jumatatu, Dkt. Kiptoo ameelezea dharura ya kupanua JKIA hadi kuufanya kuwa uwanja wa kisasa.
Ameongeza kuwa uwanja wa JKIA uliojengwa mwaka wa 1978 ulilenga kuhudumia abiria milioni 5-7 kwa mwaka.
Kwa wakati huu, uwanja huo unahudumia zaidi ya abiria milioni 10, hali inayolemaza utoaji huduma ipasavyo kwa uwanja huo ambao ni kitovu cha usafiri wa anga Afrika Mashariki.