Mbunge wa Nambale Geoffrey Mulanya, ametoa wito kwa wizara ya elimu kutoa fedha za shule kwa wakati, kuhakikisha shughuli za masomo hazitatizwi.
Kulingana na Mulanya, ucheleweshaji huo umewalazimu walimu kuwarudisha nyumbani wanafunzi na hivyo kudumaza masomo ya wanafunzi hao.
“Nataka kumwomba waziri wa elimu Ezekiel Machogu atoe fedha za shule kwa wakati, ili kufanikisha ununuzi wa vifaa vya masomo na kuendeleza miradi ya shule,” alisema Mulanya.
Aliyasema hayokatika Shule ya Sekondari ya St Mary’s DEB Nambale, wakati wa hafla ya kutoa fedha za kufadhili masomo ya wanafunzi katika eneo la Nambale.
Mulanya alitoa wito kwa wanafunzi hao kutia bidii masomoni ili kupata matokeo mazuri.
Wakati huo huo mbunge huyo aliahidi kuwasilisha hoja bungeni,kuunga mkono mpango wa lishe shuleni.
Viongozi walioandamana na mbunge huyo ni pamoja na mkurugenzi wa elimu kaunti ndogo ya Nambale Sarah Ayumba na naibu kamishna wa kaunti hiyo Carolyne Nyanchoka.