Wizara ya Afya imetangaza kupunguzwa kwa muda wa kuwalipa wawasilishaji bidhaa za afya, hadi siku 90 kutoka siku 100.
Hata hivyo, wawasilishaji bidhaa hizo wanahimizwa wahakikishe ubora wa bidhaa hizo na pia kujiepusha kuziuza kwa bei ya juu kufuatia kupunguzwa kwa muda huo.
Akiongea leo Jumatatu kwenye kongamano la wadau wa halmashauri ya usambazaji wa bidhaa tiba, KEMSA, Waziri wa Afya Susan Nakhumicha alikariri azima ya wizara hiyo ya kufufua halmashauri hiyo kufikia viwango vya kabla ya janga la virusi vya korona.
Waziri aliionya KEMSA dhidi ya utoaji zabuni kwa njia isiyofaa za usambazaji bidhaa za kiafya. Alisema serikali inatekeleza juhudi za kulipa madeni yote yaliyosalia ili kuiwezesha KEMSA kudumisha ushirikano mwema na wawasilishaji bidhaa.
Kadhalika, aliwahimiza wasambazaji bidhaa kujiepusha kutafuta mbinu za mkato kujipatia zabuni za KEMSA kwani shughuli zote zitalainishwa.
Kwenye kongamano hilo la kwanza lililoandaliwa na KEMSA, wawasilishaji bidhaa na wadau wengine walikusanyika kwenye chuo cha mafunzo ya bima kushauriana kuhusu kuiimarisha halmashauri hiyo ili kuboresha utoaji huduma.