Wizara ya Afya yafafanua kuhusu ajali inayodaiwa kuhusisha Waziri Duale

Ufafanuzi huo unajiri saa chache baada ya habari kusambaa mitandaoni kwamba Waziri Duale alihusika katika ajali ya barabarani huko Kisumu.

Marion Bosire
1 Min Read
Aden Duale - Waziri wa Afya

Wizara ya Afya imetoa taarifa ya kufafanua zaidi kuhusu ajali iliyotokea huko Kisumu inayodaiwa kumhusisha Waziri wa Afya Aden Duale.

Kulingana na taarifa hiyo, msafara wa Duale ulisimama tu katika eneo la ajali huko Otonglo karibu la kiwanda cha molasi ambapo Waziri mwenyewe alihamasisha kundi la uokoaji.

Taarifa hiyo inaelezea kwamba Duale alijipata katika eneo la tukio kwani alikuwa anaelekea katika uwanja wa ndege wa Kisumu kutoka Rarieda.

“Kufuatia ajali hiyo, mipango ya uokoaji ilianzishwa mara moja, ambapo watu 19 waliojeruhiwa walipelekwa katika hospitali ya rufaa na mafunzo ya Jaramogi Oginga Odinga,” ilielezea taarifa hiyo.

Watu wawili wanaripotiwa kufariki kwenye ajali hiyo huku mhasiriwa mmoja akifariki akipelekwa hospitalini.

Wahudumu wa dharura, maafisa wa serikali ya eneo hilo na wahudumu wa afya walichukua hatua za haraka kusaidia waathiriwa wa ajali hiyo wanaoendelea kupokea matibabu.

“Wizara ya Afya inatuma salamu za pole kwa familia za walioaga dunia katika ajali hiyo na kuwatakia afueni ya haraka wote waliojeruhiwa,” ilimalizika taarifa hiyo.

Ufafanuzi wa wizara ya Afya unajiri saa chache baada ya habari kusambaa mitandaoni kwamba Waziri Duale alihusika katika ajali ya barabarani huko Kisumu.

Share This Article