Wizara ya Afya na shirika la Amref Africa, zimeshirikiana katika kufanikisha utoaji wa huduma za afya ya msingi hapa nchini.
Ushirikiano huo unaangazia kuharakisha mitandao ya utoaji huduma ya afya ya msingi, kuboresha utumizi wa dijitali katika mifumo ya afya ya jamii, kuimarisha ushirikishi salama wa kemikali, kushughulikia magonjwa yaliyotelekezwa, kuimarisha mawasiliano kuhusu afya na masomo ya kidijitali.
Hayo yalisemwa leo Ijumaa na Katibu katika Wizara ya Afya Mary Muthoni,alipokutana na ujumbe kutoka Amref ukiongozwa na Mkurugenzi wa shirika hilo hapa nchini Dkt. Meshack Ndirangu, kukadiria maendeleo na kuwiainisha maeneo ya ushirikiano.
“Mkutano huo pia ulichunguza utekelezaji wa Mfumo wa Kenya wa Ubora wa Afya (KQMH), ukiangazia ufanisi ulioafikiwa, changamoto zilizoshuhudiwa na kuimarisha ubora wa huduma za afya katika viwango vyote vya mifumo ya afya,” alisema Muthoni.
Kwenye mkutano huo, Muthoni alikariri kujitolea kwa wizara hiyo kuendelea kushirikiana na wadau ili kuhakikisha mfumo bora wa afya unaowanufaisha watu.