Taarifa ya Jonathan Musau
Vifo vya Wakenya 69 waliofariki kufuatia mafuriko nchini vingeepukika iwapo serikali ya kitaifa na zile za kaunti zingeweka mikakati ya mapema ya kuzuia na ya kukabiliana na mafuriko.
Ndio kauli ya Waziri wa Mipangilio ya Miji na Masoko katika kaunti ya Machakos Nathaniel Nganga anayesema matayarisho ya mapema ya kukabiliana na mafuriko katika kaunti hiyo yamesaidia kutoshuhudiwa kwa kisa chochote cha kifo jinsi ilivyoshuhudiwa miaka iliyopita hususan maeneo ya Mavoko na Tala.
Nganga aidha ametoa wito kwa serikali za kaunti nchini kujiandaa mapema kukabiliana na mafuriko hasa katika kaunti zinazoathirika pakubwa kunaposhuhudiwa mvua kubwa.
Anasema usafishaji wa mabomba ya kusafirisha majitaka na uzoaji wa taka ni muhimu katika kuzuia mafuriko.