Wito wa kutunza mahakama ya ukoloni ya Kinyahwe kama kituo cha urithi wa Mau Mau

Lydia Mwangi
3 Min Read

Kaunti ya Nyandarua ni miongoni mwa maeneo yaliyozalisha wapigania uhuru wengi, lakini kwa masikitiko makubwa, wengi wao walifariki bila kutambuliwa ipasavyo, na wale waliobaki hai wanaishi katika hali ya kusahaulika kabisa.

Ahadi ya serikali ya kutambua kujitolea kwa wapiganaji wa Mau Mau haijatimizwa kikamilifu, huku kukiwa na changamoto nyingi ambazo bado hazijapatiwa suluhisho, zikiwemo ukosefu wa makumbusho rasmi na msaada kwa mashujaa waliosalia hai.

Katika kijiji cha Gĩtĩrĩ, Kinangop, ndani ya kaunti ya Nyandarua, tunakutana na Kihiko Kibue Nyota na Wahinya Gakinyi, miongoni mwa wapiganaji wachache wa Mau Mau waliobaki hai. Mioyo yao imeelemewa na uchungu, kwani licha ya kujitolea kwao, juhudi za serikali kuwakumbuka na kuwaheshimu wapiganaji wa Mau Mau kama wao zimekuwa hafifu, na hivyo kujihisi kusahaulika.

Safari yao katika harakati za kupigania uhuru haijarekodiwa vyema wala kutambuliwa kwa upana, na sasa wanaitaka serikali ijitokeze si tu kuwasadia katika siku zao za mwisho, bali pia kutambua mchango wao rasmi.

Mandhari ya milima na mapango ya kina ya Nyandarua yalikuwa sehemu muhimu za kujificha kwa wapiganaji wa Mau Mau wakati wa mapambano, lakini hadi leo, mipango ya kuyafanya maeneo hayo kuwa kumbukumbu au alama za kihistoria haijatekelezwa.

Chemchemi za maji ambazo zilihifadhi maisha wakati wa vita bado hazijatunzwa, hali inayoakisi kusahaulika kwa historia yenye nguvu.

Sasa, wapigania uhuru hawa wanatoa wito kwa serikali kuanzisha eneo la kumbukumbu katika Mahakama ya Kikoloni ya zamani ya Kinyahwe, na kuibadilisha kuwa kivutio cha kihistoria kwa ajili ya ukumbusho na elimu.

Mahakama hii ilikuwa ngome ya kikoloni ambapo wapiganaji wengi wa Mau Mau walifunguliwa mashtaka na kuhukumiwa wakati wa harakati za kupigania uhuru.

Kubadilisha Kinyahwe kuwa kituo cha Urithi wa Mau Mau kutakuwa ishara ya heshima kwa wale waliopigania uhuru wa Kenya, mahali pa kutafakari kitaifa, kujifunza, na hatua ya kuelekea kutimiza ahadi ya “kutosahau kamwe” gharama ya uhuru wetu.

Gavana wa Nyandarua, Kiarie Badilisha, ameonyesha utayari wa kushirikiana na serikali kuu katika kutimiza ndoto hii, na sasa ni wakati mwafaka wa kuifanya ndoto hii ya urithi kuwa halisi. Na kuifanya Kinyahwe isisimame tena kama alama iliyosahaulika ya dhuluma za ukoloni, bali iwe kumbukumbu ya fahari kwa wanawake na wanaume jasiri waliotoa maisha yao kwa ajili ya nchi tunayoifurahia leo.

Lydia Mwangi
+ posts
Share This Article