Chama cha Wiper kimeunga mkono taarifa ya rais wa chama cha wanasheria nchini LSK Eric Theuri, ile ya Daktari Fred Ojiambo mwenyekiti wa chama cha mawakili wa hadhi ya juu na ya kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga kuhusu matamshi ya Rais Ruto dhidi ya idara ya mahakama.
Kiongozi wa chama hicho Kalonzo Musyoka alitoa taarifa kwa vyombo vya habari ambapo alihimiza idara ya mahakama isitishwe na yeyote hata serikali kuu na iendelee kutekeleza majukumu yake ya kuhakikisha haki za wakenya zinalindwa.
Kulingana naye wasioheshimu utawala wa kisheria sasa wanajionyesha hadharani.
Kalonzo anasema iwapo kuna maafisa wa idara ya mahakama wamehusika kwenye ufisadi zipo taratibu za kufuata ili kuwashughulikia ilivyoainishwa kwenye sheria ya huduma za mahakama ya mwaka 2011.
Alitaja hatua ya mahakama ya upeo ya siku sita zilizopita ya kutupilia mbali kesi ya rufaa ya jaji Said Chitembwe na kusumisha uamuzi wa jopo kazi lililobuniwa kumchunguza.
Kikao cha majaji watano wa mahakama ya upeo kilishikilia kwamba Chitembwe aliondolewa afisini kuambatana na sheria.
Kiongozi huyo mwenza wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya anasema wanaunga mkono mpango wa chama cha LSK wa kuandaa maandamano ya amani kote nchini wiki ijayo ili kuunga mkono utawala wa sheria na kusimama na idara ya mahakama.