Wizara ya Masuala ya Vijana, Sanaa na Michezo kwa ushirikiano na asasi nyingine za serikali imezindua wiki ya kitaifa ya vijana mwaka 2023.
Uzinduzi huo uliofanyika katika bewa kuu la Chuo Kikuu cha Nairobi, uliongozwa na Waziri Ababu Namwamba.
Akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi, Namwamba alisema wizara yake inaandaa mswada wa maendeleo ya vijana kwa nia ya kuwainua kiuchumi huku ikiunda sera ambazo zitahakikisha kwamba vijana wanajumuishwa kwenye ngazi zote serikalini.
Wiki ya vijana itaangazia mpango wa kiuchumi wa serikali ya Kenya Kwanza almaarufu Bottom-up Economic Agenda -BETA pamoja na malengo endelevu.
Mazungumzo kuhusu namna vijana wanaweza kuwa maajenti wa mabadiliko katika nyanja hii kupitia sera na sheria pia yataandaliwa kwenye hafla hiyo ya wiki nzima.
Mandhari ya mwaka huu ni “Ujuzi wa Kijani kwa Vijana: kwa dunia endelevu” na vijana watapata fursa ya kuonyesha bidhaa, ubunifu na ujuzi wao kwenye “Hustla bazaa”.
Wiki ya kitaifa ya vijana mwaka huu itaandaliwa kati ya tarehe 7 na 11 mwezi huu na itafikia kilele kwa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya vijana mwaka 2023, Agosti 12.