WHO yasambaza vifaa tiba kabla ya msimu wa mvua

Tom Mathinji
1 Min Read
Shirika la WHO latoa vifaa vya matibabu vya thamani ya shilingi milioni 9.7 katika kaunti tano hapa nchini.

Kaunti tano hapa nchini zimenufaika na vifaa vya matibabu kutoka kwa Shirika la Afya Duniani, WHO kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua za vuli.

Vifaa hivyo vya thamani ya shilingi milioni 9.7, vinalenga kuimarisha matayarisho ya kukabiliana na changamoto za kiafya ambazo huenda zikasababishwa na mvua hiyo.

Kaunti hizo zinajumuisha Kilifi, Homa Bay, Mandera, Turkana na Kajiado.

Kulingana na WHO, vifaa hivyo vinatarajiwa kuwafaidi watu 164,600 katika maeneo hayo ambayo hukumbwa na magonjwa yanayosababishwa na maji.

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa imeonya kuwa sehemu kadhaa za taifa hili zitashuhudia mvua za vuli kuanzia mwezi Oktoba hadi Disemba.

Kulingana na utabiri huo, mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu na nne ya mwezi Oktoba katika eneo la kati ya nchi na Nairobi.

Vile vile, viwango vya maji katika maziwa ya bonde la ufa vinatarajiwa kuwa vya juu, na huenda vikasababisha mafuriko.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article