Mzozo unaoendelea nchini Sudan unaongeza changamoto za afya ambazo tayari zinashuhudiwa na hali ya njaa nchini humo.
Katibu Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus anasema mahitaji ya watu nchini humo ni mengi, upatikanaji wa huduma za afya unasalia kuwa mgumu mno, na hali zilizosababishwa na mzozo huo zinaongeza hatari ya magonjwa ya mlipuko kusambaa na kuua watu.
Mzozo huo umeongeza kwa kiwango kikubwa idadi ya watu wanaokabiliwa na hatari ya njaa kutoka milioni 11.7 hadi milioni 19.1.
“Mzozo unaoendelea, yakiwemo mashambulizi dhidi ya wahudumu wa afya, hospitali, uchukuzi na bidhaa, unazuia manusura wa dhuluma za kijinsia kupata huduma muhimu za matibabu wakati wanazihitaji zaidi. Wanawake na wasichana wanapaswa kutozuiliwa kupata huduma wanazohitaji, hasa manusura wa dhuluma za kijinsia na wanawake wanaohitaji usaidizi wakati wa ujauzito hadi wajifungue. Wafanyakazi wa afya na hospitali ni lazima zilindwe,” alisema Tedros wakati akiwahutubia wanahabari juu ya masuala ya afya duniani leo Jumatano.
“Njia za usafirishaji wa bidhaa za kibinadamu na afya zinapaswa kulindwa.””
WHO imethibitisha visa 50 kupitia Mfumo wake wa Uangalizi wa Mashambulizi Yanayofanywa dhidi ya Hospitali tangu kuanza kwa mgogoro huo mnamo mwezi Aprili.
Visa hivyo vinajumuisha 32 vinavyohusisha hospitali, vifo 10 na majeruhi 21 vilivyoripotiwa miongoni mwa wafanyakazi wa afya na wagonjwa.