Wetang’ula ahimiza wakazi wa eneo la kati kuunga mkono serikali ya Rais Ruto

Marion Bosire
1 Min Read

Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula amehimiza wakazi wa eneo la katikati mwa nchi kuendelea kuunga mkono kwa dhati serikali ya Rais William Ruto.

Akizungumza katika eneo bunge la Mwea, Wetang’ula alitambua jukumu muhimu lililotekelezwa na jamii ya eneo hilo katika kuunda serikali ya Kenya Kwanza huku akiwashauri wasikubali kuyumbishwa na siasa za mgawanyiko.

Alikuwa akihutubia waumini katika kanisa la Mtakatifu Peter Claver huko Mwea ambapo alisisitiza haja ya kukataa viongozi wanaojaribu kugawanya watu kwa misingi ya kikabila.

Alisema umoja waliodhihirisha wakati wa kampeni unafaa kuendelea kwa ajili ya maendeleo na ufanisi wa nchi na wawe macho dhidi ya viongozi wanaopendekeza umoja kwa maslahi finyu yanayoacha nje jamii zingine.

Kuhusu kanisa, spika huyo alisisitiza umuhimu wake katika kuhimiza umoja wa kitaifa na akawataka viongozi wa dini kuendelea kuombea nchi hii.

Jambo lingine alilozungumzia Wetang’ula ni familia ambayo alitaja kuwa nguzo muhimu ya umoja nchini akisema bunge litaendelea kuratibu sheria za kulinda maadili ya kifamilia.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *