Makala ya 34 ya fainali za kombe la mataifa ya Afrika AFCON yatang’oa nanga Jumamosi, kwa mchuano wa ufunguzi wa kundi A kati ya wenyeji Ivory Coast dhidi ya Guinea Bissau kuanzia saa tano za usiku.
Ivory Coast wanashiriki AFCON kwa mara ya 25 likiwa taifa la pili kushiriki fainali nyingi baada ya Misri wanaoshiriki kwa mara ya 26 mwaka huu na watakuwa wakiwania ubingwa kwa mara ya tatu.
Guinea Bissau watakuwa wakicheza AFCON kwa mara ya 4, lakini wamekuwa wakiburura mkia katika makala matatu waliyoshiriki awali.
Shirika la KBC litapeperusha mubashara mechi zote 52 za kindumbwendumbwe hicho kutoka Ivory Coast kati ya Januari 13 na Februari 11 mwaka huu.
Kaimu Mkurugenzi wa KBC Paul Macharia akizungumza wakati wa uzinduzi wa Ijumaa, ameahidi kuwapa Wakenya burudani kabambe ya AFCON kupitia kwa Idhaa zote za redio na pia Runinga ya Y254 na KBC Channel 1.