Idadi kubwa ya Wakenya wanaunga mkono kubuniwa kwa afisi ya kiongozi wa upinzani.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kampuni ya Trends and Insights For Africa (TIFA).
Kulingana na utafiti huo, asilimia 45 ya waliohojiwa wanaunga mkono kubuniwa kwa afisi hiyo huku asilimia 17 wakisema hawana pingamizi na kubuniwa kwa afisi hiyo.
Asilimia nyingine 21 ya waliohojiwa inapinga vikali kubuniwa kwa afisi ya kiongozi wa upinzani.
Wengine asilimia 13 hawapingi wala kuunga mkono kubuniwa kwa afisi ya kiongozi wa upinzani.
Rai William Ruto alipendekeza kubuniwa kwa afisi hiyo katika waraka wake kwa bunge la kitaifa kabla ya kuundwa kwa kamati ya mazungumzo ya maridhiano ya kitaifa.
Hata hivyo, aslimia 48 ya waliohojiwa wanahisi kuwa upinzani utafifishwa ikiwa utakubali afisi hiyo wakati asilimia nyingine 36 wakiamini upinzani utakuwa imara zaidi ukipata afisi hiyo.
Watu wengine asilimia 16 hawaamini ikiwa kuundwa kwa afisi hiyo kutabadilisha chochote.
Utafiti huo uliandaliwa kati ya Septemba 8 na 10 mwaka huu na kuwashirikisha watu 1,007 waliohojiwa.