Wendy Williams aelezea kilichompeleka hospitali

Alifanyiwa uchunguzi wa akili na kulingana na ripoti alipatikana kuwa sawa kabisa.

Marion Bosire
2 Min Read

Wendy Williams ambaye alikuwa mtangazaji wa redio na ambaye pia aliwahi kuendesha kipindi chake cha mahojiano kwenye runinga, ameelezea kuhusu kilichompeleka hospitalini maajuzi.

Williams alihojiwa kwa njia ya simu kwenye kipindi kiitwacho “The View” ambapo alisema kwamba alihitaji hewa safi nje ya makazi ya wanaougua maradhi ya akili anakoishi.

Alisema alitolewa damu kwenye tezi kwa ajili ya vipimo na akaamua pia kufanyiwa uchunguzi huru wa kiakili.

Mtangazaji huyo wa zamani amekuwa chini ya usimamizi ulioagizwa na mahakama tangu mwaka 2022 kufuatia kile kilichotajwa kuwa ugonjwa wa akili usio na tiba.

Aliwahi kuathirika na utegemezi wa pombe na dawa za kulevya awali lakini anasema sasa anaweza kuishi maisha yake vizuri tu bila pombe.

Baada ya kutoka hospitalini, Wendy na mpwa wake wa kike walikwenda kupata chajio kabla yake kurejea kwenye makazi hayo ya kusaidiwa.

Taarifa ya wakili wa msimamizi wa kisheria wa Wendy ilisomwa kwenye kipindi cha The View na ilielezea kwamba aliwekwa chini ya usimamizi huo na jaji ambaye alimtaja kuwa asiyeweza kujisimamia kutokana na ugonjwa wa dementia.

Kinyume na madai ya Wendy, wakili huyo alisema kwamba anaruhusiwa kutagusana na watu wa familia yake na anapata huduma nzuri za afya katika makazi yake.

Williams anasema huwa haruhusiwi kuonana na watu wa familia yake na hana ugonjwa wa akili inavyodaiwa huku akitaka kuondolewa chini ya usimamizi huo wa kisheria.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *